Kwa miaka mingi, Skype ilikuwa kama daraja lililounganisha marafiki walio mbali mkubwa kijografia, familia zilizotawanyika katika mabara tofauti, na hata wanahabari waliotegemea mahojiano ya moja kwa moja kutoka sehemu.
Ilikuwa chombo kilichobadilisha jinsi watu walivyowasiliana,
ikitoa nafasi kwa mazungumzo ya video kwa mara ya kwanza katika historia ya
mawasiliano ya mtandaoni.
Lakini, kama ilivyo kwa kila kizazi cha teknolojia, muda wa
Skype ulikuwa unayoyoma polepole. Microsoft, mmiliki wa huduma hiyo, hatimaye
imetangaza kuwa mwezi Mei utakuwa mwisho wa safari ndefu ya Skype.
Uamuzi huu, kama ilivyokuwa kwa simu za mezani za kuzungusha zilizopitwa na wakati, umeacha wengi wakiwa na hisia mseto baadhi wakiwa na huzuni ya kuagana na huduma waliyoitumia kwa zaidi ya miongo miwili, huku wengine wakiwa tayari wameshasonga mbele na teknolojia mpya kama Microsoft Teams, WhatsApp, na Zoom.
Mwaka 2003, Skype ilizaliwa ilikuwa kama muujiza wa
mawasiliano huduma iliyotoa nafasi kwa mtu yeyote kupiga simu za video bila kulazimika kulipa gharama
kubwa za kimataifa. Ilikuwa zama ambapo kufanya mawasiliano ya umbali mrefu
bado kulihitaji kadi za simu na gharama kubwa kwa kila dakika uliyoongea. Skype
ilibadilisha yote haya kwa kutoa mawasiliano kupitia intaneti, ikitoa fursa kwa
watu kuongea kwa kuonana uso kwa uso
kupitia skrini ya kompyuta.
Katika miaka yake ya dhahabu, Skype ilikuwa kila mahali.
Familia zilizoishi mbali na ndugu zao
waliweza kuwasiliana kwa urahisi. Waandishi wa habari waliweza kufanya
mahojiano ya moja kwa moja na wageni wao. Hata makampuni makubwa yalitegemea
Skype kwa mikutano yao ya biashara.
Lakini kama ilivyo kwa teknolojia nyingine nyingi, ushindani
ulikuwa mkubwa na kuzizima teknolojia za zamani. Simu za mkononi zilianza kuwa
na huduma za video, na programu kama FaceTime, WhatsApp, na Zoom zilianza
kuchukua nafasi yake polepole. Wakati huo huo, Microsoft ilizindua Microsoft
Teams mwaka 2017, ikilenga soko la biashara na elimu. Janga la COVID-19
lilipokuja, ilichanua kama ua lenye maji ya kutosha shule, makampuni,
na hata mashabiki wa michezo walihamia huko kwakufanya mikutano na mijadala ya moja kwa moja.
Hatimaye, Microsoft ikaamua ni wakati wa kuachana na Skype na kuwekeza nguvu zote katika Teams.
Kwa watumiaji waaminifu wa Skype, tangazo hili limekuja kama
mshangao na pigo kubwa. Hata hivyo, wengine ambao ni wafanya kazi wa makampuni
ya teknolojia, wanasema hawashangazwi na uamuzi huu.
Microsoft inatoa fursa kwa wale waliokuwa wakitumia Skype kuhifadhi mazungumzo yao ya zamani na kuhama kwenda Teams, lakini wengi wanahisi kuwa hii ni dalili nyingine ya jinsi teknolojia zinavyozidi kukua.
Kama ilivyokuwa kwa Windows Phone na teknolojia nyingine nyingi ambazo zilikuwa kubwa lakini zikafutwa kutokana na maendeleo mapya, Skype sasa inaelekea mwishoni.
Lakini je, ni kweli kwamba haina nafasi tena? Labda kwa
wapenzi wa teknolojia za zamani, Skype itaendelea kubaki kwenye kumbukumbu zao
kama sehemu ya historia ya mawasiliano. Kama vile mtu anavyoweza kuweka simu ya
zamani ya mzunguko kama ukumbusho wa enzi zilizopita, Skype itabaki katika
akili za wengi kama nyota iliyowaka kwa muda mrefu, kabla ya mwanga wake
kuzimwa na mawimbi mapya ya teknolojia.
Kwa sasa, tunasema kwaheri kwa Skype programu iliyoleta
mapinduzi ya mawasiliano, lakini hatimaye ikashindwa na kasi ya maendeleo. Kumbuka Mwisho wa enzi moja, na mwanzo wa nyingine.

0 Comments