"Marehemu Ruge aliwahi kusema Ogopa Mungu na Teknolojia"
Katika ulimwengu wa kidijitali, taarifa zako za kibinafsi
zinaweza kuangukia mikononi mwa watu wasio waaminifu ikiwa taarifa au vitu
vyako havijafutika kikamilifu kupitia simu au kompyuta.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2023 ya Shirika la Data
Security Council of India, zaidi ya asilimia 40 ya vifaa vilivyotupwa bila
kufutwa data kikamilifu vilikuwa na taarifa za siri za watumiaji, jambo ambalo
linaweza kusababisha uhalifu wa mtandaoni.
Je, Umewahi Kufikiria Vitu Unavyofuta Kwenye Kifaa Chako
Huenda Wapi?
Wataalamu wa teknolojia wanasema, hakuna kitu kinafutika
ulimwenguni hasa katika upande wa teknolojia ...
Yaani kivipi? Mfano umepiga picha ya kitu ukasema umekifuta
kwenye simu yako, picha hiyo haiwezi kuonekana tena, lakini bado inahifadhiwa
kwenye hifadhi ya ndani ya kifaa chako, unaambiwa wataalamu wa mambo wanauwezo
wa kukirudisha endapo wakipata Access ya kifaa yako. Hii ndiyo sababu kuna
programu maalumu zinazoweza kurejesha vitu vilivyofutwa.
Swali la kujiuliza kwa Nini Faili Hazifutiki Moja kwa
Moja?
Sababu kuu ni ufanisi. Simu au Kompyuta yako haiondoi faili au data zilizofutwa moja kwa moja, kwa sababu mchakato huo unahitaji muda mrefu zaidi.
Badala yake nafasi inabaki wazi kwa matumizi mapya ya data
nyingine. Njia hii pia inatoa fursa ya kurejesha vitu vilivyofutika kwa bahati
mbaya.
Lakini hali hii ipo tofauti katika mfumo wa HDD yaani
(Hard Disk Drive) na SSD (Solid State Drive).
Vitu vilivyofutwa kupitia HDD (HARD DISK DRIVE)
vinaweza kurejeshwa kwa urahisi kwa kutumia programu za urejeshaji data.
Hata hivyo kupitia mfumo wa SSD (Solid State Drive),
hali ni tofauti. SSD hutumia mchakato maalum unaoitwa TRIM, ambao
unafuta data mara moja ili kuboresha kasi na ufanisi wa kifaa. Katika hatua
nyingine, bado kuna hatari ya baadhi ya data kutofutika kikamilifu endapo
haitosimamiwa kwa umakini.
Ikiwa unataka kuhakikisha kuwa vitu vyako vimefutwa kabisa
na haviwezi kurejeshwa kupitia kifaa unachotumia, ni muhimu kutumia programu
maalum za kufuta data kama vile Eraser, CCleaner, au Darik’s Boot and Nuke
(DBAN).
Programu hizi hufanya kazi ya kuandika data mpya juu ya
nafasi iliyoachwa wazi na vitu vilivyofutwa, na hivyo kufanya data za awali
zisirejeshwe tena. Ili kuhakikisha usalama wa data zako, tumia mbinu za
kitaalamu za kufuta data. Usalama wa taarifa zako ni jukumu lako.
Tafakari mara mbili kabla ya kufuta, kwa kufanya hivyo,
utakuwa umelinda faragha yako na kuzuia uwezekano wa taarifa zako kutumiwa
vibaya.

0 Comments