MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA YA BIOMETRIC

Fikiria dunia ambayo utambulisho wako hauhitaji kadi, nywila au hata saini. Bali alama zako za vidole, sura au hata sauti yako. Hii si ndoto tena, bali ni hali halisi inayoendelea kushika kasi duniani, ikiendeshwa na teknolojia ya biometric.

Teknolojia hii imepata mafanikio makubwa, hususani nchini China, ambayo imeunganishwa na mifumo ya kisasa kama kamera za usalama (CCTV) na huduma za kidijitali. Mojawapo ya matumizi yake ni katika kuboresha huduma  za  Social Credit System, mfumo unaolenga kupima na kuboresha tabia za kijamii na kiuchumi za raia wake.

Mfumo huu hutumia taarifa za alama za vidole kuhakiki utambulisho (BIOMETRIC) Kwa lengo la kupunguza udanganyifu, kurahisisha huduma kuanzia ulipaji wa bidhaa mpaka manunuzi, pamoja na kuboresha usalama kwa umma.

Faida zake ni dhahiri zipo wazi, Wahenga wanasema kizuri hakikosi kasoro licha ya mfumo huu kupata mafanikio bado unakumbwa na changamoto hasa kwa mataifa yanayoendelea kama Tanzania.

Swali la kujiuliza, Je tuko tayari kuboresha mfumo huu au tunahitaji muda zaidi?

Katika mazingira yetu, swali kubwa linalojitokeza ni usalama wa taarifa za kibinafsi. Katika nchi nyingi zinazoendelea, mifumo ya kuhifadhi na kulinda taarifa za kidijitali bado ni dhaifu, na mara nyingi haina uwazi wa kutosha kuhusu jinsi data za watu zinavyotumika.

Je, tunayo miundombinu madhubuti ya kuhakikisha taarifa hizi haziingiliwi na watu wenye nia mbaya, ikiwemo sheria na sera zinazolinda faragha ya raia?

Kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la International Telecommunication Union (ITU) mwaka 2022, nchi nyingi zinazoendelea bado zina safari ndefu kufikia kiwango kinachoridhisha cha usalama wa data.

Hili linaibua mjadala mzito kuhusu uwezo wa mataifa haya kushiriki kikamilifu katika mapinduzi ya teknolojia hii.

TUSIFANYE HARAKA.

Ni kweli, teknolojia ya biometric inaweza kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo. Lakini je, tunapaswa kuikimbilia bila mpango madhubuti? Ili teknolojia hii iwe na manufaa ya kweli, tunahitaji muda wa kujifunza, kuboresha miundombinu yetu, na kuimarisha sera zinazolinda haki za watu.

Hii si hadithi ya kutisha, bali ni changamoto ya kufikirisha. Dunia ya biometric hipo hapa, lakini swali ni moja, Je Tanzania na mataifa mengine yanayoendelea yamejiandaa kuingia katika ulimwengu huu pamoja na uwajibikaji unaohitajika?  Ni wakati wa kufanya maamuzi sahihi, si kwa haraka, bali kwa busara. Wakati teknolojia ikisonga mbele, faragha ya binadamu lazima ibaki kuwa kipaumbele.

Post a Comment

1 Comments